Siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kukabidhiwa ripoti ya pili ya kuchunguza mchanga wa dhahabu wa Kampuni ya Madini ya Acacia, wananchi wa Tarime wamevamia mgodi wa North Mara kwa siku mbili mfululizo.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni mwendelezo wa kupinga uonevu unaofanywa na wawekezaji hao kupitia Kampuni ya Acacia.
Taarifa kutoka wilayani Tarime zinadai kuwa wananchi hao walivamia mgodi huo juzi saa 2.00 usiku na jana asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao walikwenda hadi kwenye mtambo wa kufua dhahabu na kufanya uharibifu huo kabla ya kudhibitiwa na jeshi la polisi.
Hata hivyo shuhuda huyo ambaye hakutaka kutaja jina , alisema vurugu hizo zimetokana na uongozi wa Kampuni ya Acacia kushindwa kuwalipa fidia wananchi waliokuwa na maeneo yao tangu awali.
Alisema wakati madini yalipogundulika, wananchi walioondolewa walitathiminiwa mali zao yakiwamo mashamba, nyumba na kuahidiwa kulipwa fidia akini hadi sasa hawajalipwa stahiki zao.
Alisema kwa siku mbili mfululizo wanachi wenye madai yao walifika katika ofisi za kampuni na kuona baadhi ya majina ya wanaotakiwa kulipwa fidia yakiwa yamebandikwa katika ubao wa matangazo lakini majina ya wengine yakiwa hayajabandikwa.
