Watu watano wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa doria. Taarifa ya polisi imesema watu hao waliuawa walipojaribu kuwavamia wafanyabiashara wa madini katika machimbo ya Mwime nje kidogo ya Mji wa Kahama.
Watuhumiwa pia wanadaiwa kuhusika na mauaji ya viongozi wa Serikali ya Mtaa, polisi na wanasiasa mkoani Pwani katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Simon Haule amesema kwamba, watu hao walijeruhiwa usiku wa kuamkia jana katika eneo la Mwanva katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, walipokabiliana ana kwa ana na polisi waliofika eneo hilo.
Kamanda Haule amesema baada ya polisi kufika kwenye eneo la tukio, watu hao walijificha kwenye mashimo yanayotumiwa kuchimba mchanga na kuanza kurushiana risasi na askari.
Amesema katika mapambano hayo, watuhumiwa walizidiwa nguvu na kujeruhiwa na walifariki dunia walipokuwa njiani kupelekwa hospitali.
