Hotuba Ya Mhe. Waziri Mkuu Aliyoitoa Alhamis Bungeni

In Kitaifa

UTANGULIZI

 1.Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani – CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum – CHADEMA. Pia, Taifa lilimpoteza Mheshimiwa Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu imekumbwa na majanga na maafa yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu awajalie nafuu ya haraka wale wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa amani wale waliopoteza maisha, Amina! Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki. Pia ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata ajali ya kugongwa na pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone haraka na aweze kurejea Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.

PONGEZI NA SHUKRANI

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wao. Sisi tunaowasaidia tunajivunia uongozi wao mahiri, uzalendo uliotukuka na dhamira njema waliyonayo kwa Watanzania.
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limepokea na kuwaapisha Wabunge wapya watano, ambao ni Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb.), Mheshimiwa Anne Killango Malecela (Mb.), Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb.), Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) na Mheshimiwa Salma Rashidi Kikwete (Mb.). Ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wapya kwa heshima waliyoipata ya kujumuika nasi kwenye Bunge hili. Kama ilivyo ada, tutatoa ushirikiano unaotarajiwa kwa Waheshimiwa Wabunge hawa ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na tija. Kipekee, ninampongeza Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Pia ninatumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu wapya walioteuliwa na Mheshimiwa Rais yaani Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Dk. Leonard Akwilapo, Maimuna Tarishi na Dk. Ave Maria Semakafu. Nawapongeza sana wote walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.
 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ninawashukuru kipekee sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, niwapongeze Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa Kamati zao wakati wa kupitia makadirio ya sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mafungu yote.
 1. Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.
 1. Mheshimiwa Spika, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Mbunge wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.), Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) kwa ushirikiano wao mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya wakati akiitumikia nafasi hiyo. Ninamtakia kazi njema kwenye jukumu lake  jipya la kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani. Vilevile, ninawashukuru wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Eric F. Shitindi na aliyekuwa Katibu Mkuu Bwana Uledi A. Mussa kwa ushauri wao wa kitaalam kwangu na kwa Waheshimiwa Mawaziri.
 1. Mheshimiwa Spika, ninazishukuru pia nchi marafiki, Taasisi na Mifuko ya Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Madhehebu ya Dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga uchumi wa nchi yetu. Misaada na mikopo iliyopatikana kwa wakati imechangia kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
 1. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono na kuielewa vizuri dhamana ya Kitaifa niliyonayo ya kusimamia utendaji wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mwisho ninaishukuru familia yangu hususan mwenza wangu mpendwa, Mary na watoto wetu kwa upendo, dua na kuendelea kunitia moyo ili nitekeleze kwa ufanisi zaidi majukumu yangu ya Kitaifa. Asanteni sana!
 2. MWELEKEO WA BAJETI

  1. Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Katika kipindi hicho, yapo mambo mengi yaliyofanyika kwa mafanikio makubwa ambayo yataanishwa kwa kina katika bajeti za Sekta pindi Mawaziri husika watakapoziwasilisha. Baadhi ya mafanikio hayo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Elimu Bila Malipo; kuongezeka kwa uzalishaji na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini; kuimarika uwajibikaji na nidhamu katika Utumishi wa Umma; kuongeza ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma; kuboresha huduma za kiuchumi na za kijamii; na kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Serikali, Watumishi wa Umma na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake, kwani bila ushirikiano wao, tusingeweza kupata mafanikio hayo.
  1. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuandaliwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; ahadi za Mheshimiwa Rais alizotoa wakati wa Kampeni, pamoja na maelekezo yake wakati anazindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015. Bajeti hii itaendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka uliopita na kushughulikia utatuzi wa vikwazo vya kukuza uchumi kwa haraka na baadhi ya changamoto zilizojitokeza. Aidha, Serikali itajikita zaidi katika maeneo yatakayochangia kuimarisha uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za jamii. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufikia azma hiyo ili dhamira yetu ya kuboresha maisha ya Watanzania iweze kutimia. Ni vyema tukakumbuka kwamba tuna mwaka mmoja tu wa utekelezaji wa yale tuliyopanga kufanya ndani ya kipindi cha miaka mitano. Tutatumia bajeti ya mwaka ujao wa fedha kukabili changamoto zilizojitokeza. Ahadi ya Serikali ni kuendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na bila ubaguzi wowote, huku tukitanguliza mbele maslahi ya Taifa.

  SERIKALI KUHAMIA DODOMA

  1. Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi, alitangaza uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Kufuatia uamuzi huo, mipango ya kuhamia Dodoma kwa awamu ilianza baada ya mahitaji halisi yatakayoiwezesha Serikali kuhamia Dodoma kubainishwa, ikiwa ni pamoja na ofisi na nyumba za makazi kwa viongozi na watumishi wa umma. Awamu ya kwanza ilipangwa kuhama ifikapo mwisho wa mwezi Februari, 2017.
  1. Mheshimiwa Spika, ninafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari watumishi 2,069 wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi wengine wamekwishahamia Dodoma kama ilivyopangwa. Vilevile, Wizara zote zimepata majengo ya Ofisi yatakayotumika katika kipindi cha mpito.

  Mheshimiwa Spika, ili Mji wa Dodoma uweze kuendelezwa kwa mpangilio mzuri, Serikali inaupitia upya Mpango Kabambe wa Mji wa Dodoma. Mapitio hayo yatasaidia sana kuepuka makosa yaliyofanyika katika miji mingi hususan ujenzi holela unaochangia katika uchafuzi wa mazingira na kuharibu mandhari ya miji. Ni wazi kwamba, ujenzi wa Mji wa Dodoma hautafanywa na Serikali pekee, bali tutaendelea kuhamasisha Sekta binafsi na

  1. wadau wengine kuwekeza Dodoma. Ninalipongeza sana Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kujenga nyumba 300 za makazi hapa Dodoma ambazo watumishi wanaweza kununua au kupangishwa. Ninatoa wito kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja, kuboresha miundombinu na kudhibiti ujenzi holela kwa kushirikiana kwa karibu na Manispaa ya Dodoma na Taasisi nyingine za Serikali.

  SIASA

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, hali ya kisiasa nchini imeendelea kuwa shwari na ya kuridhisha. Aidha, Chaguzi Ndogo zilifanyika tarehe 22 Januari, 2017 katika Jimbo la Dimani – Zanzibar na Udiwani katika kata 20 Tanzania Bara kwa kushirikisha wagombea kutoka vyama 15 vya siasa. Ninavipongeza vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo, na kipekee nakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa Jimbo la Dimani na viti 19 vya udiwani katika chaguzi hizo.
  1. Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mashauri 53 ya kupinga ushindi wa Ubunge na mashauri 194 ya kupinga ushindi wa Udiwani yalifunguliwa. Mashauri hayo yamekwishasikilizwa na hukumu kutolewa, isipokuwa shauri moja la kupinga matokeo ya Ubunge katika Jimbo la Mbagala. Nizipongeze Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuhakikisha kesi hizo zinaendeshwa kwa kasi na kwa weledi na hivyo kuwezesha wananchi kuendelea kupata uwakilishi.
  1. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini, hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa kote nchini kujenga utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa za kuunganisha watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi.

  MUUNGANO

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kudumisha muungano wetu ambao ni tunu na mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima. Wananchi wanaendelea kunufaika na matunda ya Muungano wetu ambao ni imara na dhabiti. Serikali zote mbili zinafanya mashauriano kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, viongozi na watendaji wa sekta nyingine zisizo za Muungano wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu na kubaini maeneo ya ushirikiano kwa ustawi wa wananchi wa pande zote mbili. Jumla ya vikao 13 vya sekta ambazo siyo za Muungano vilifanyika kati ya Julai 2016 na Machi 2017.
  1. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendesha kwa ufanisi mkubwa kikao kilichofanyika tarehe 13 Januari, 2017 ambapo taarifa kuhusu hoja zilizopatiwa ufumbuzi, maagizo na maelekezo ya kufuatilia utekelezaji wa changamoto zilizobaki ilitolewa. Serikali itaendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wetu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
  2. HALI YA UCHUMI

   1. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa viashiria vya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2016/2017 vinaonesha kuwa uchumi wetu unakua na kuimarika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia asilimia 7.0 mwaka 2016. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa kwenye ukuaji huo ni uchimbaji madini na mawe; usafirishaji na uhifadhi wa mizigo; habari na mawasiliano; pamoja na shughuli za fedha na bima. Mfumuko wa Bei uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja na kasi ya upandaji bei ilipungua kutoka wastani wa asimilia 6 mwaka 2015 hadi asilimia 5.2 mwaka 2016. Kwa upande mwingine, tathmini ya hali ya Taasisi za Fedha inaonesha kuwa Benki zetu ziko salama na zina mitaji na ukwasi wa kutosha. Aidha, taarifa za Mashirika mbalimbali ya Kimataifa zinaonesha kwamba katika mwaka 2016 uchumi wa Taifa letu ulikua vizuri na hivyo kutufanya kuwa miongoni mwa nchi sita (6) za Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeweka juhudi kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kutokana na juhudi hizo, makusanyo ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliongezeka kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 850 kwa mwezi katika mwaka 2015/2016 hadi Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwezi katika mwaka 2016/2017. Pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, juhudi kubwa zimefanyika kudhibiti matumizi ya rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu, wizi na upotevu wa fedha za umma. Mwenendo huo umeiwezesha Serikali kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa kwa fedha za ndani na pia utoaji huduma kwa wananchi. Serikali itaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kila anayestahili kulipa kodi aweze kuilipa.
   1. Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa viashiria vya uchumi wa nchi yetu katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni dalili njema katika kujenga uchumi imara na tulivu utakaotusaidia kuelekea katika Uchumi wa Viwanda na kufikia nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Serikali itaongeza juhudi katika kuchochea ukuaji wa sekta za kipaumbele zenye fursa kubwa ya kukuza uchumi kwa haraka na kuondoa umaskini kama vile Kilimo na Viwanda. Pia, itahakikisha kwamba sekta wezeshi kama vile Nishati, Habari na Mawasiliano, Fedha na ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara, bandari, reli, vivuko na viwanja vya ndege zinaimarishwa. Vilevile, Serikali itaendelea kuhimiza utekelezaji thabiti wa miradi ya maendeleo na kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji.

   Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwezesha Wananchi kupitia Mipango na Programu mbalimbali kwa kuelekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Serikali imeweka mazingira bora kwa vikundi vya kiuchumi na vijana kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, SACCOS na VICOBA. Aidha, Serikali imeanzisha majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika mikoa yote na kufanya mapitio ya Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa mwaka 2007. Mapitio hayo yana lengo la kuboresha uendeshaji na usimamizi wa Mfuko huo ili kuwezesha wanawake wengi zaidi kukopesheka.

   Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Hivyo, Serikali inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi ili

   1. kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi. Katika mwaka 2016/2017, Serikali inatoa mafunzo kwa vijana 9,120 katika fani mbalimbali zikiwemo stadi za kushona nguo, kutengeneza bidhaa za ngozi, mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi na mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za kujiajiri katika fani mbalimbali. Jumla ya vijana 1,469 wamehitimu mafunzo hayo na kupata ajira. Vijana 7,651 waliobaki wanaendelea kupata mafunzo kupitia viwanda vya TOOKU GARMENTS, MAZAVA FABRICS, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), VETA na Don Bosco. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itatoa mafunzo ya kukuza ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 15,350 katika fani mbalimbali.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kwa vikundi vya vijana 297 katika Halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia mapato yake ya ndani zimetoa Shilingi bilioni 4.6 ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana 2,356. Hatua hizi zimekwenda sanjari na utengaji wa maeneo maalum yenye jumla ya ekari 85,603 kwa ajili ya shughuli za vijana za kilimo, biashara ndogo ndogo, burudani na michezo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kusimamia Halmashauri zote nchini kutenga asilimia tano (5) ya mapato yao kwa ajili ya vijana na asilimia tano (5) kwa wanawake.

   Ajira na Mahusiano Mahali pa Kazi

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa juhudi za kukuza ajira nchini kama inavyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Hadi kufikia Machi 2017, jumla ya ajira 418,501 zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 239,017 sawa na asilimia 57 zimezalishwa katika sekta binafsi wakati ajira 179,484 sawa na asilimia 43 zimezalishwa kutokana na shughuli za sekta ya umma ikiwemo miradi ya maendeleo.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 58 ya migogoro ya kikazi inatokana na kutozingatiwa kwa taratibu za kuachisha kazi. Sekta zinazoongoza kwa migogoro ya kazi ni usafirishaji, ujenzi, ulinzi binafsi, elimu, huduma za hoteli na viwanda. Katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, Serikali imefanya kaguzi na kusimamia uundwaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi. Aidha, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi imeendelea kutimiza wajibu wake wa kusuluhisha migogoro ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari 2017, Tume imesajili jumla ya migogoro 8,832 kati ya hiyo migogoro 3,319 sawa na asilimia 37.6 ya migogoro yote iliyosajiliwa imesuluhishwa. Kati ya migogoro hiyo iliyosuluhishwa, migogoro 1,957 ilifikia suluhu (mediation) na migogoro 1,362 haikufikia suluhu. Aidha, migogoro 5,513 inaendelea kusuluhishwa katika hatua mbalimbali.  

   Ninatoa wito kwa waajiri na waajiriwa wote nchini, kuzingatia Sheria za Kazi na kuimarisha uhusiano mzuri kwenye maeneo ya kazi, ili muda mwingi zaidi utumike kwenye uzalishaji mali badala ya kutatua migogoro. Vilevile, ni muhimu sana kuimarisha kaguzi za kazi na kuendelea kusaini mikataba ya kuunda na kusajili mabaraza ya wafanyakazi ili kuimarisha zaidi mahusiano mahali pa kazi.

   MAENDELEO YA KISEKTA

  3. Sekta za Uzalishaji

   Viwanda

   1. Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Viwanda vinavyopewa kipaumbele ni vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa nchini na nje ya nchi. Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini. Natoa pongezi kwa Bodi na Menejimenti ya Mifuko hiyo, kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa viwanda nchini. Aidha, ninaendelea kuyasisitiza mashirika ya umma kuhakikisha kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda.

   Maliasili na Utalii

   1. Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ni moja kati ya sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Kote ulimwenguni, mafanikio ya sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa hutegemea miundombinu thabiti ya utalii, huduma bora na ulinzi na usalama. Ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo, Serikali inaboresha miundombinu ya utalii, kupanua wigo wa vivutio vipya vya utalii na kuimarisha huduma ya usafiri wa anga. Vilevile, Serikali inafanya juhudi kubwa za kudhibiti ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ambapo watuhumiwa 897 walitiwa mbaroni na kati yao watuhumiwa 282 wamefikishwa Mahakamani.
   1. Mheshimiwa Spika, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi watalii 1,284,279  mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 12 na kuliingizia Taifa Dola za Marekani bilioni 2. Juhudi zilizoanza za kuliimarisha shirika letu la ndege zinalenga pia kutoa mchango mkubwa kwenye sekta ya utalii kwa kusafirisha watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi. Shabaha yetu ni kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu na pia mapato yatokanayo na sekta hiyo. Nitumie fursa hii kuisihi sekta binafsi kuwekeza zaidi kwenye miundombinu muhimu ya sekta hii zikiwemo hoteli, kuboresha huduma na kubuni mbinu mpya za kuvutia watalii.

   Kilimo

   1. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ikijumuisha mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka ulifikia tani 16,172,841 ikilinganishwa na mahitaji ya kitaifa ya tani 13,159,326. Hivyo, katika kipindi hicho nchi ilikuwa na ziada ya tani 3,013,515 za chakula. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017, hali ya upatikanaji wa mvua katika Mikoa inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha ukame na upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Tathmini ya awali imebainisha kwamba Halmashauri 55 zimeathirika na ukame.

   Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula kutoka katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Aidha, wafanyabiashara waliokuwa wamehifadhi nafaka katika maghala, walitakiwa kuzisambaza katika masoko ya ndani. Vilevile, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walielekezwa kuwahamasisha na kuwaelekeza wakulima kupanda mbegu bora za mazao ya kilimo yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa muda mfupi kwa

   1. kipindi hiki cha mvua za masika. Ili kutoa msukumo katika kazi hiyo, kiasi cha tani 1,969 za mbegu bora za mazao yanayostahimili ukame zilinunuliwa na Serikali na kusambazwa katika Halmashauri zilizobainika kuathirika na ukame. Pia, wakulima wanaendelea kuhamasishwa kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa kupanda mazao hayo yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.
   1. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wetu, Serikali imeweka dhamira ya kuongeza uzalishaji, tija na kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifanikisha kupatikana kwa tani 277,935 za mbolea na tani 23,333 za mbegu bora. Aidha, hadi Februari 2017, Serikali ilitoa tani 30,773 za mbolea ya ruzuku ya kukuzia na kupandia kupitia vituo vya mauzo ya mbolea vya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).
   1. Mheshimiwa Spika, moja ya ahadi ya Serikali kwa wakulima wetu ni kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali zinazochangia kupunguza faida kwa mkulima. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifuta baadhi ya tozo za mazao ambazo ni kero kwa wakulima katika mazao ya pamba, chai na kahawa. Tozo zilizofutwa kwenye zao la pamba ni mchango wa Mwenge wa Shilingi 450,000 unaotolewa na kila kiwanda cha kuchambua Pamba na ada ya vikao vya Halmashauri za Wilaya ambayo ni shilingi 250,000. Kwa zao la chai, kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na katika zao la kahawa, ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 nayo pia imefutwa.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeboresha Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani kwa kuanzisha utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada. Mathalani, katika msimu wa 2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya zao la korosho nchini. Aidha, Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani na utaratibu wa minada umeongeza ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hususan nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya kutegemea soko la India pekee. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na uchambuzi wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha mkulima, mvuvi na mfagaji anufaike zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri zetu. Kwa sasa, tunashughulikia zao la tumbaku kwa kupitia tozo zake na pia kubaini ubadhirifu unaoendelea kwenye ushirika huo.

   Mifugo

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza uzalishaji wa mitamba na uhimilishaji wa mifugo ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa na wenye tija. Mitamba 546 imezalishwa kutoka mashamba ya Serikali na mitamba 88 kutoka NARCO na kusambazwa kwa wafugaji wadogo. Aidha, Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji – NAIC Usa River, Arusha kimeimarishwa na kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za ng’ombe hadi kufikia dozi 10,494 ikilinganishwa na dozi 8,000 zilizozalishwa na kusambazwa katika mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390 mwaka 2015/2016 hadi ng’ombe 457,557 mwaka 2016/2017.

   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha kituo chetu cha kuzalisha mitamba cha Kitulo wilayani Makete ili kukiongezea uwezo wake. Aidha, Serikali inatoa nafasi kwa mashamba binafsi kuzalisha mitamba zaidi kama mashamba ya ASAS kule Iringa ili wafugaji wadogo wanufaike.  Serikali pia itaendelea na 

   1. zoezi la kutenga, kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji na kujenga miundombinu ya mifugo kwa kuongeza idadi ya malambo na mabwawa katika mikoa. Hatua hizo zitasaidia kupunguza uzururaji wa mifugo na migogoro baina ya wafugaji na wakulima na hifadhi za misitu.

   Madini

   1. Mheshimiwa Spika, Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wetu. Serikali imetenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kutoa ruzuku pamoja na kuimarisha shughuli za ugani. Katika kipindi cha mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imetenga maeneo 11 yenye ukubwa wa hekta 38,567 kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo. Maeneo hayo ni Msasa na Matabe mkoani Geita, Biharamulo na Kyerwa mkoani Kagera, Itigi mkoani Singida, D-Reef, Ibindi na Kapanda Mkoani Katavi, Ngapa mkoani Ruvuma, Kitowelo na Namungo mkoani Lindi pamoja na Nzega mkoani Tabora.
   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali za madini na kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini kwa migodi mikubwa, ya kati na midogo. Aidha, Serikali itaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani wa madini hayo.

   Huduma za Kiuchumi

   Ardhi

   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi ya ujenzi wa mfumo huo awamu ya kwanza ilizinduliwa rasmi Agosti, 2016 na Mkandarasi tayari ameanza kazi. Sambamba na zoezi hilo, Serikali inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi. Kukamilika kwa mradi huo kutaboresha utendaji kazi, kuharakisha huduma za utoaji hati miliki, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi ambapo nyaraka zote za ardhi zitakuwa katika mfumo unganishi wa kielektroniki.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliidhinisha ramani za upimaji zenye jumla ya viwanja 78,771 na mashamba 239. Aidha, Serikali imekamilisha upigaji wa picha za anga za Jiji la Dar es Salaam na inaendelea kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi  baina ya wakulima, wafugaji na hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini.
   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kujenga Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi na kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi kwa kufanya mapitio ya Sera na Sheria za Ardhi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sera, sheria, kanuni na miongozo ya ardhi ili kudhibiti viashiria vya migogoro ya matumizi ya ardhi nchini. Ninatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashughulikia migogoro ya ardhi mapema na kuweka mazingira wezeshi ya upimaji wa ardhi katika Halmashauri zao.

   Umeme

   Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua thabiti za kuongeza uzalishaji, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji umeme. Katika 

   1. mwaka 2016, umeme uliozalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa uliongezeka na kufikia Gigawatt hours (GWh) 7,092 ikilinganishwa na Gigawatt hours (GWh) 6,227 zilizozalishwa mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 9. Vilevile, Serikali imepanua na kuboresha njia za usafirishaji umeme kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 400 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kutoka Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Wakala ulikamilisha ujenzi wa vituo sita (6) vya kuongeza nguvu ya umeme kutoka msongo wa kilovolti 11 hadi kilovolti 33 katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru; ujenzi wa njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilometa 17,740 za msongo wa kilovolti 33; ujenzi wa vituo vidogo vya kupoza na kusambaza umeme 4,100; na ujenzi wa njia ndogo ya usambazaji umeme wenye urefu wa kilometa 10,970.
   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme nchini. Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Kabaale (Uganda) hadi Tanga (Tanzania). Serikali pia, itawezesha uwekaji wa mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwenye viwanda na matumizi ya majumbani pamoja na uendelezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas – LNG)mkoani Lindi.

   Barabara

   1. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imejenga na kukarabati jumla ya kilometa 430 za barabara kuu sawa na asilimia 62 ya lengo la kilometa   Aidha, ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya TAZARA unaendelea vizuri pamoja na maandalizi ya kuitisha zabuni za ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze kwa kiwango cha Expressway. Vilevile, ujenzi wa barabara za juu (Interchange) kwenye makutano ya Barabara ya Ubungo ulizinduliwa rasmi tarehe 20 Machi, 2017. Hizi ni hatua muhimu za kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015.

   Vivuko na Usafiri Majini

   1. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali ilipanga kujenga kivuko kipya cha Pangani (MV Pangani) na kukarabati kile cha Magogoni – Kigamboni. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba hadi kufikia Februari, 2017 ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo ulikuwa umekamilika. Aidha, ununuzi wa boti ndogo za abiria kwa ajili ya vivuko vya Kilambo – Namoto (Mtwara), Mkongo – Utete (Pwani), Pangani – Bweni (Tanga) na Msemo – Msangamkuu (Mtwara) utakamilika katika mwaka huu wa fedha. Kwa upande wa huduma za usafiri kwenye maziwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa meli moja katika Ziwa Victoria, meli mbili katika Ziwa Nyasa zitakazofanya safari kati ya Kyela na Mbambabay pamoja na ukarabati wa meli za MV Victoria na Butiama (Ziwa Victoria) na MV Liemba (Ziwa Tanganyika).

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Bandari nchini kwa kufanya upanuzi na kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Mifumo ya Ulinzi katika bandari hizo imeimarishwa na mashine za kisasa za kukagua mizigo zimefungwa. Kutokana na jitihada hizo, tumeanza kuona mwelekeo mzuri wa kuimarika ufanisi wa kiutendaji hususan katika Bandari ya Dar es Salaam. Tutaendelea kufanya maboresho zaidi ili Bandari ya Dar es Salaam iwe chaguo namba moja katika usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi yetu.   

   Reli

   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Reli ya Kati ili kuongeza uwezo wa reli hiyo kutoa huduma za uchukuzi nchini na nchi jirani zinazotumia bandari zetu. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli mpya ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kiwango cha standard gauge imeanza kutekelezwa kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha reli ya Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 205). Taratibu za kuwapata makandarasi wa ujenzi wa reli kutoka Morogoro – Makutupora (kilometa 336), Makutupora- Tabora (kilometa 294), Tabora- Isaka (kilometa 133) na Isaka- Mwanza (kilometa 254) zinaendelea.

   Usafiri wa anga

   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imetekeleza kwa dhati azma ya kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Katika kipindi hicho, ndege mbili (2) aina ya Dash 8 – Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zilinunuliwa na kuanza kutoa huduma mwezi Oktoba, 2016. Aidha, mwishoni mwa mwaka 2016, Serikali iliingia mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine nne (4). Kati ya hizo, ndege moja ya aina ya Dash 8 – Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2017. Ndege nyingine mbili (2) aina ya CS300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila moja zinatarajiwa kuwasili mwezi Juni, 2018 na ndege kubwa moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2018.
   1. Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ununuzi wa ndege hizi kutaisaidia ATCL kuongeza safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuchangia katika jitihada za kuongeza watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio vyetu na kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. Aidha, ATCL imeanzisha safari za kuja Dodoma na hivyo kuongeza uhakika wa usafiri wakati huu ambapo Serikali inahamia Dodoma. Wigo wa upanuzi kwa viwanja vyote nchini unaendelea na sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.

   Mawasiliano

   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kutekeleza Mradi wa Anuani za Makazi na Postikadi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centrekitakachorahisisha utoaji wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za kibenki. Aidha, Sekta ya Mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi waVideo Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika Mikoa 26 na Taasisi za Serikali.

   Mheshimiwa Spika, Serikali pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano Vijijini kwa kushirikiana na Kampuni   ya   Viettel   ya   Vietnam.   Mradi huu 

   1. unatekelezwa kwa kipindi cha  miaka  mitatu 2015-2017. Viettel wamekwishafikisha miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417, Ofisi za Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za Posta 68.  
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre). Lengo ni kuongeza na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Pamoja na ujenzi wa vituo hivyo, matumizi ya TEHAMA yameongezeka na hivyo kuziwezesha taasisi za Serikali kutoa mchango mkubwa kwenye uboreshaji na utoaji wa huduma, kuongeza mapato na kuokoa gharama mbalimbali.

   Sekta ya Huduma za Jamii

   Elimu

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa walimu wa shule za msingi kwa kuwapa mafunzo hasa katika ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Jumla ya walimu 22,995 wa shule za msingi na walimu 519 wanaofundisha elimu maalum kwa wanafunzi wasioona na wenye ulemavu wa kusikia wamepewa mafunzo hayo. Lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayemaliza darasa la saba anajua kusoma na kuandika.
   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila malipo. Tangu utekelezaji wa mpango huo uanze, Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa Shilingi bilioni 18.77 kila mwezi, ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na mpango huo. Mpango huo umeleta manufaa kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini na cha kati na umeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwenye shule za Msingi na Sekondari. Kufuatia ongezeko hilo, tulijikuta tukilazimika kupambana na upungufu wa madawati, jambo ambalo liliifanya Serikali ianzishe kampeni maalum ya kumtoa sakafuni mtoto wa Kitanzania. Hivi sasa madawati sio tatizo tena kwenye shule nyingi nchini. Nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa Watanzania wote walioshirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya upungufu wa madawati. Natoa pongezi kwa taasisi binafsi, watu binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao yote.
   1. Mheshimiwa Spika, uchumi wa viwanda kwa kiasi kikubwa unahitaji rasilimaliwatu yenye weledi hasa katika masomo ya hisabati na sayansi. Kama zilivyo nchi nyingine Barani Afrika, Tanzania inakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kutopenda kusoma masomo ya hisabati na sayansi na hivyo kuchangia katika ufaulu duni kwenye masomo hayo. Ni dhahiri kuwa watoto wetu wasipoweka bidii katika masomo ya hisabati na sayansi viwanda vyetu vitalazimika kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi jambo litakalowafanya Watanzania kuwa watazamaji.

    Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imefanya juhudi za kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi katika ngazi zote za shule. Aidha, Serikali inaendelea na Mpango wa Ujenzi wa Maabara katika shule za sekondari na vyuo vikuu pamoja na ununuzi wa vifaa. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imenunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule 1,625 za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara na usambazaji wa vifaa umeanza mwezi Machi, 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017 kwa nchi nzima. Aidha, 

   1. Serikali inatoa mafunzo kwa walimu 5,920 wanaosoma Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA kwa shule za Sekondari. Serikali inaendelea na mpango wake wa kujenga maabara za kompyuta ili wanafunzi wawe na uelewa wa TEHAMA. Utekelezaji wake utafanyika hatua kwa hatua.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa vibali vya ajira kwa walimu wa Hisabati na Sayansi 4,129. Natoa wito kwa wazazi wenzangu kuhamasisha watoto wetu kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi. Naagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau wengine waandae Mkakati Maalum wa kuhamasisha na kuwavutia wanafunzi kusoma masomo ya Hisabati na Sayansi. Mkakati huo pia uwezeshe upatikanaji wa walimu watakaofundisha masomo ya Hisabati na Sayansi katika shule za msingi na sekondari kwa kipindi kifupi bila kuathiri ubora wa ufundishaji.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam. Ujenzi wa majengo 20 ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 Vilevile, Serikali inaimarisha miundombinu katika vyuo vya ufundi vya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya na Chuo cha Ufundi Arusha kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya Ufundi na Sayansi nchini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuwezesha upatikanaji wa wataalam mahiri katika nyanja mbalimbali hususan Sayansi na Teknolojia.

   Maji

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kusogeza huduma za maji karibu zaidi na wananchi ili wasitumie muda mwingi kutafuta maji badala yake wajikite katika shughuli za uzalishaji mali. Ili kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini ikiwemo miradi ya vijiji 10 chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kati ya mwezi Julai na Desemba 2016, miradi 90 ya maji vijijini ilikamilika na kufanya idadi ya miradi iliyokamilika kufikia 1,301 kati ya miradi 1,810 Miradi 509 iliyobaki ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na yote inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni, 2017.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini katika Halmashauri zote nchini ukiwemo mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe unaolenga kuhudumia wananchi zaidi ya 456,000 katika vijiji 38 kwenye miji ya Same, Mwanga na Korogwe Vijijini. Ili utoaji wa huduma ya maji uwe endelevu, wananchi waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya maji. Nitumie fursa hii kuwakumbusha watendaji katika Halmashauri zote kusimamia kikamilifu sheria inayokataza shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.

   Afya

   Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ikiwemo kuhimiza lishe bora. Aidha, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya na tiba pamoja na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba 

   1. imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Vilevile, Serikali imeanzisha utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama. Serikali pia imeanzisha maduka ya dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu kwa wananchi katika hospitali za mikoa ambapo hadi sasa maduka manane (8) yameanzishwa, na ujenzi wa maduka mengine katika mikoa iliyobakia unaendelea.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaimarisha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto nchini kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto wa mwaka 2016-2020. Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya vituo vya Afya nchini vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa matatizo ya uzazi ikiwemo upasuaji na huduma za watoto wachanga. Hadi sasa, vituo vya afya 159 vinatoa huduma za upasuaji ambapo vituo 106 ni vya Serikali.

   Vilevile, Serikali imeimarisha utoaji wa huduma za kinga na hivyo kuchangia kutokomezwa kwa ugonjwa wa Polio hapa nchini na hatimaye nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizopatiwa hati ya kutokomeza ugonjwa huo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi na kuimarisha huduma za kinga ili kupunguza vifo vya watoto na akina mama pamoja na makundi mengine. Naomba nitoe wito kwa wote Watanzania wajiunge kwa wingi na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili Serikali iweze kuwachangia kupitia mfumo huo.

   BUNGE

   1. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Katika mwaka 2016/2017, Ofisi ya Bunge iliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano mitatu ya Bunge ambapo maswali 1,054 ya kawaida, nyongeza na ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa. Miswada kumi (10) ya Sheria ilijadiliwa na kupitishwa na Bunge. Aidha, Bunge liliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano ya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa huduma za Hansard, utafiti, utawala na kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa Ofisi ya Bunge. Ofisi ya Bunge pia ilisimamia kazi ya ukarabati wa jengo la Bunge pamoja na kuratibu ujenzi wa Ofisi za Waheshimiwa Wabunge. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba kama kawaida.

   MAHAKAMA

   1. Mheshimiwa Spika, utendaji wa mhimili wa Mahakama nchini umezidi kuimarika. Katika mwaka 2016/2017, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 279,331 kati ya 335,962 katika ngazi zote za Mahakama sawa na asilimia 83.1 ya mashauri yote. Pamoja na kazi kubwa ya kusikiliza mashauri, Mahakama imesogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kukamilisha ukarabati na ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. Pia, kazi za ukarabati wa Mahakama Kuu katika Mkoa wa Mbeya inaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Kibaha Mkoa wa Pwani umekamilika na kuzinduliwa.

   Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba, katika mwaka 2017/2018, Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani. Hata hivyo, ili Mahakama ifanye kazi zake vizuri, shughuli za upelelezi wa kesi na uendeshaji wa mashtaka zinatakiwa pia kuimarishwa zaidi. Serikali 

   itafanya kila liwezekanalo kuimarisha taasisi zote zinazohusika katika mlolongo wa utoaji haki ili wananchi wapate haki zao kwa wakati.

   MASUALA MTAMBUKA

   Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali

   1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliahidi kuanzisha Mfumo wa Wazi wa Kielektroniki wa kufuatilia uwajibikaji na utendaji Serikalini. Mfumo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za Serikali kwa kuwawezesha Viongozi kutoa maelekezo na kufuatilia utekelezaji wake. Aidha, Mfumo huo utasaidia ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ahadi na Maagizo ya Mheshimiwa Rais na Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Napenda kulialifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mfumo huo umekamilika, kuzinduliwa rasmi na mafunzo kutolewa kwa wataalamu katika Wizara zote. Mfumo huo pamoja na mambo mengine utaongeza kasi ya utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za Serikali kwa wakati na pia kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma. Wizara na Taasisi zote za Serikali zinatakiwa kuutumia Mfumo huo kikamilifu ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Serikali na kusaidia viongozi kutatua vikwazo pale vinapojitokeza.

   Vita dhidi ya Rushwa

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba, 2015 zimetambulika hata na Mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa Duniani. Taarifa ya Shirika laTransparency International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016 imeonesha kuwa viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini.
   1. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2016/2017, Serikali kupitia TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa mahakamani. Kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU, kiasi cha Shilingi bilioni 9.75 Katika Mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na mapambano yake dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

   Vita dhidi ya UKIMWI

   1. Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya UKIMWI yamekuwa yakitegemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo. Ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ulioanzishwa na Serikali miaka miwili iliyopita, ulizinduliwa tarehe 01 Desemba, 2016 ambapo kupitia harambee iliyofanyika kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo, shilingi milioni 347 zilipatikana kama ahadi. Vilevile, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa huduma kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) ambapo hadi Desemba, 2016 WAVIU 839,574 sawa na asilimia 63 ya WAVIU wote, walikuwa wamepatiwa dawa. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwahamasisha WAVIU kujitokeza na kuingia kwenye Mpango wa Tiba ya Kufubaza Athari za UKIMWI. Aidha, Serikali imekamilisha uandaaji wa miongozo minne ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ikijumuisha Mpango Kazi wa Kinga, Mkakati wa Kondomu, Mkakati wa Uwekezaji na Mpango kazi wa jinsia.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2017/2018, itaimarisha uratibu wa afua za UKIMWI kwa wadau wote wa sekta ya umma na binafsi na kupitia mifumo ya uratibu iliyoanzishwa. Serikali kwa kushirikiana na wadau pia itazijengea uwezo Kamati zilizo katika ngazi ya jamii hususan vijiji na kata ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kupunguza na kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia mfumo ulio katika jamii. Vilevile, Serikali itakamilisha utafiti wa nne wa kubainisha viwango vya maambukizo ya UKIMWI nchini na kuboresha ushiriki wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi katika kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI.

   Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu

   1. Mheshimiwa Spika, katika 2016/2017, Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji. Aidha, Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali pia inahakikisha kwamba watumiaji wa lugha ya alama wanapata haki ya kupata habari na vituo vyote vya televisheni vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya alama. Napenda kuvikumbusha Vituo vya Televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo vyao. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya kufundishia.

   Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya

   1. Mheshimiwa spika, dawa za kulevya zinaathiri maisha ya vijana wetu wengi na hivyo kuzima ndoto za maisha yao na kupunguza nguvu kazi ya Taifa. Ili kupambana na janga hilo, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Marekebisho hayo yameipa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nguvu ya kukamata, kupeleleza na kushitaki watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Watendaji Wakuu watakaosimamia Mamlaka hiyo.

   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Januari, 2017 watuhumiwa 11,303 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya katika sehemu mbalimbali nchini. Kati ya watuhumiwa hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa 

   1. mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea. Ni imani yangu kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya itaendeleza kwa kasi zaidi juhudi za kupambana na uingizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini. Watanzania wana imani kubwa na Mamlaka hii na ninaomba wote tuipe ushirikiano wakati wote kwani vita hii ni kubwa na ni ya Kitaifa! Aidha, nawasihi wazazi wenzangu, tuwe karibu na vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili wasiingie kwenye mtego huu wa dawa za kulevya.

   Uratibu wa Maafa

   1. Mheshimiwa Spika, Serikali wakati wote inahakikisha kuwa nchi ipo katika hali ya utayari wa kukabiliana na maafa na pia kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo huduma za matibabu, ushauri wa kisaikolojia, na vifaa pale maafa yanapotokea. Serikali imejenga vituo vipya 20 vya upimaji wa hali ya hewa  katika Halmashauri 11 za Tarime, Nyamagana, Muleba, Longido, Geita, Maswa, Kigoma, Sikonge, Kongwa, Serengeti, na Kahama. Kuwepo kwa vituo hivyo kutaongeza ufanisi katika upatikanaji wa taarifa za tahadhari hasa kwa majanga ya mafuriko na ukame.
   1. Mheshimiwa Spika, kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa mwezi Septemba 2016, Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua za kushughulikia athari zilizotokana na tetemeko hilo. Huduma za afya na tiba na za kibinadamu za chakula na malazi zilitolewa kwa walioathirika. Vilevile, Serikali ilirejesha hali ya miundombinu iliyobomoka, yakiwemo majengo ya Serikali na Taasisi za Umma 686, Kituo cha wazee Kilima pamoja na kutoa maturubai 6,237, mahema 367, mabati 7,300 na mifuko ya saruji 1,825 kwa walioathirika. Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule za Ihungo, Nyakato na Omumwani pamoja na ukarabati wa Kituo cha afya Kabyaile Ishozi. Ninapenda kuwashukuru sana wananchi wote na wadau waliotoa michango yao kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.

   HABARI NA MICHEZO

   Habari

   1. Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 ambayo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini. Kanuni za Sheria hiyo zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika. Natoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na kanuni hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za kijamii.

   Maendeleo ya Michezo

   Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona dalili nzuri za kuimarika kwa shughuli za michezo hapa nchini. Mathalan, timu ya Mpira wa Miguu ya Serengeti Boysimefuzu kushiriki Mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika Gabon, Mei 2017. Napenda nimshukuru sana Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amewaaga na kuwakabidhi bendera ya Taifa tayari kwenda kushiriki vita hiyo. Nawaomba Watanzania wote tuungane pamoja kuiombea na kuiunga mkono timu yetu kwa michango ya hali na mali ili kuiwezesha kushiriki kikamilifu. Kwa upande wa riadha, Mtanzania mwenzetu Alphonce Simbu alipata medali 

   1. katika mbio za marathon huko Mumbai nchini India. Aidha, mwezi Septemba 2016, Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji la CECAFA. Ninatoa pongezi kwa wale wote walioliletea Taifa sifa kupitia michezo. Naziombea dua ili ziweze kushiriki michuano ya kimataifa.
   1. Mheshimiwa Spika, michezo ni sekta muhimu katika kuongeza ajira, kuimarisha afya, kukuza uchumi, kuimarisha umoja wa Kitaifa na kuitangaza nchi Kimataifa. Nchi nyingi zilizofanikiwa kimichezo ziliwekeza zaidi kujenga vipaji vya vijana katika michezo. Natoa wito kwa TFF ihakikishe kuwa vijana wa Timu ya Serengeti Boys wanawekewa Mpango Endelevu wa Kukuza Vipaji Vyao na kutunzwa vyema ili waweze kuiwakilisha nchi yetu katika mashindano mengine ya kimataifa. Aidha, vyama vingine vya michezo vitoe msukumo mkubwa kwenye kuwekeza zaidi kwa vijana wa shule za msingi na sekondari kwani hao ndio watakuwa wawakilishi wetu katika miaka ijayo. Na mwaka huu, michezo ya shule za msingi na sekondari itarejea na kufanyika mkoani Mwanza kama ilivyotangazwa mwaka jana. Nazisihi wizara husika za TAMISEMI na Wizara ya Elimu zianze maandalizi mapema na kuandaa mpango huo na kutoa taarifa timu hizo ziweze kujiandaa na kushindana ili tupate wachezaji imara wa kushiriki michuano hiyo.

   ULINZI NA USALAMA

   1. Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka ya nchi yetu. Serikali imeendelea kuimarisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia zana na vifaa vya kivita na kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya askari ulioanza mwaka 2013/2014. Kwa upande mwingine, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inakamilisha ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwa njia ya ubunifu katika baadhi ya Magereza ikiwemo ujenzi unaoendelea katika Gereza la Ukonga wa ghorofa 12 zenye uwezo wa kuishi askari na familia 320.
   1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kufanya operesheni za kuzuia uhalifu nchini, kufanya upelelezi wa kesi kwa kasi ili kupunguza mlundikano wa kesi zilizopo mahakamani,  na kusimamia sheria za barabarani ili kupunguza ajali zinazoleta madhara kwa wananchi. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa askari na maafisa wa jeshi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kupambana na vitendo vya rushwa na kupambana na biashara ya dawa za kulevya. 

   MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

   1. Mheshimiwa Spika, kudumisha uhusiano mzuri na mataifa mengine duniani pamoja na mashirika ya kimataifa ni moja kati ya Misingi ya Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tumeendelea kuimarisha ujirani mwema baina yetu na nchi jirani, nchi marafiki pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa, jitihada ambazo zimetuwezesha kuvutia mitaji mikubwa ya uwekezaji, utalii pamoja na kupanua fursa za kibiashara. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imefungua Balozi mpya sita (6) katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Balozi hizo zina kazi kubwa ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo. Serikali itaendelea kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi na kuweka mikakati ya kunufaika na nafasi ya nchi yetu kihistoria. Hivyo, ninatoa wito kwa mabalozi wetu wote waendelee kuitangaza nchi yetu kama eneo mwafaka lenye fursa nyingi za utalii, uwekezaji na biashara.

   HITIMISHO

   1. Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda tunahitaji nidhamu ya kazi, ubunifu, elimu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia. Vilevile, tunahitaji kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za kiuchumi na jamii na kuondoa urasimu usio wa lazima. Nafarijika kwamba misingi tunayoendelea kujenga katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda kama nilivyoeleza awali. Ili kufanya mafanikio hayo yawe endelevu, naomba nihitimishe hotuba yangu kwa kusisitiza mambo makuu yafuatayo:-
   • Mosi, ustawi wa nchi yetu na mafanikio ya mipango yetu ya maendeleo vinategemea amani na utulivu. Hivyo, kila mmoja wetu aweke nadhiri ya kuendelea kuilinda na kuienzi amani ya nchi yetu ili mipango yetu iweze kufanikiwa. Tunalo jukumu la kuhimiza amani ili tufanye kazi zetu kwenye mazingira ya amani na utulivu.
   • Pili, jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa kila mwananchi. Njia pekee ya kuijenga nchi yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kulipa kodi kwa hiari na kufichua wakwepa kodi wote na wala rushwa.
   • Tatu, ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji wananchi wenye afya njema na maarifa ya kufanya kazi na ubunifu. Tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa;
   • Nne, rasilimali tulizonazo ipo siku zitaisha. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa uangalifu ili zitufae sisi na vizazi vijavyo. Tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi hiki na vizazi vijavyo;
   • Tano, tuongeze nidhamu na uwajibikaji katika kila jambo la maendeleo tunalolifanya na kuzingatia matumizi ya muda. Tamaduni na mila zinazohamasisha uvivu na uzembe ni lazima tuzipige vita kwa nguvu zetu zote; na
   • Mwisho, dawa za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii kwa kufichua mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya. Ahadi yetu ni kuwapa ushirikiano na kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika.

   MAKADIRIO YA  MAPATO NA MATUMIZI  YA  FEDHA  ZA OFISI  YA  WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2017/2018

   1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Moja; Milioni Mia Sita Sitini na Nne, na Hamsini na Tano Elfu (Sh.171,664,055,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na Nne, Milioni Mia Sita Arobaini na Tatu, na Mia Tatu Thelathini na Tisa Elfu (Sh.74,643,339,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Tisini na Saba, Milioni Ishirini, na Mia Saba na Kumi na Sita Elfu (Sh.97,020,716,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.Vilevile, ninaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Moja, Milioni Mia sita Hamsini na Mbili na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.121,652,262,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Nne, Milioni Mia Nne Hamsini na Mbili, na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.114,452,262,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Saba na Milioni Mia Mbili (Sh.7,200,000,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. 
    1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

WANAFUNZI 500 WAPEWA MBINU WASILOWEE KWENYE MADAWA YA KULEVYA.

Na Tonie kaisoe ,Arusha Wanafunzi zaidi ya 500 wa shule ya Sekondari Arusha Jiji na Wilaya ya Arumeru wamepewa mbinu

Read More...

MR. IBU AFARIKI DUNIA

Mchekeshaji maarufu wa Nollywood nchini Nigeria, John Okafor, almaarufu Mr. Ibu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Read More...

POLISI, LATRA WAPIGA FAINI MABASI YALIYO ZIDISHA NAULI ARUSHA.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikaiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu